10 Mei 2025 - 22:03
Source: Parstoday
Ni vipi vipaumbele vya Iran katika Duru ya 4 ya Mkutano wa Mazungumzo kati ya Iran na Nchi za Kiarabu

Duru ya 4 ya Mkutano wa Mazungumzo kati ya Iran na Nchi za Kiarabu chini ya anwani "Uhusiano Imara na Maslahi ya Pande Mbili" inafanyika Doha mji mkuu wa Qatar kwa ushirikiano wa pamoja wa Baraza la Kiistratejia la Uhusiano wa Nje la Iran na Kituo cha Utafiti cha al Jazira.

Ujumbe wa Iran unashiriki katika Duru ya Nne ya Mkutano wa Mazungumzo kati ya Iran na Nchi za Kiarabu  kuanzia leo Jumamosi hadi Jumatatu Mei 12 ukiongozwa na Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje. Araqchi ameelekea Qatar kwa madhumumu ya kushiriki katika duru ya nne ya Mkutano wa Mazungumzo kati ya Iran na Nchi za Karabu baada ya ziara yake nchini Saudi Arabia. 

Mkutano huu wa Doha unafayika lengo likiwa ni kujadili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na nchi za Kiarabu; kwa kuzingatia suala hili kwamba ushirikiano huo ni wenzo muhimu kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili na pande kadhaa. Weledi wa mambo watajadili na kubadilishana mawazo kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji wa pamoja na kupanua ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, nishati, ustawi na teknolojia. 

Kikao cha ufunguzi wa mkutano huu tajwa kimefanyika leo Jumamosi kwa kuhudhuriwa na shakhsia mbalimbali watajika wanaoziwakiklisha pande mbalimbali katika Mkutano wa Mazungumzo kati ya Iran na Nchi za Kiarabu. 

Kwa upande wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mkutano kati ya  nchi za Kiarabu na Iran ni uwanja muhimu wa kuonyesha juhudi za kidiplomasia na kusisitiza dhamira yake ya mazungumzo ya kikanda. Wakati huo huo mkutano huu unaziandalia fursa nchi za Kiarabu kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Iran kuhusu masuala mbalimbali ya kieneo.

Malengo makuu ya Tehran katika mkutano huu ni pamoja na kutilia mkazo kwake kuhusu  amani na utulivu wa kikanda, kuchunguza njia mbalimbali za kupunguza mivutano katika maeneo yenye migogoro kama vile Lebanon na Syria, kupanua ushirikiano wa kiuchumi na nchi za Kiarabu, na kuweka wazi msimamo wake kama mshirika wa dhati wa majirani zake.

Washiriki wa Duru ya Nne ya Mkutano wa Mazungumzo ya Iran na Nchi za Kiarabu unaoudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu na wa kidiplomasia, watafiti mashuhur na weledi wa masuala ya kisiasa watabainisha mitazamo yao katika mkutano huo wa Doha katika mifumo ya kinadharia na ya vitendo kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kushughulikia changamoto zinazofanana, na kuimarisha ustawi endelevu.

Duru ya kwanza ya mkutano huu ilifanyika mwaka 2022 mjini Doha, Qatar chini ya anwani "Mazungumzo kwa ajili ya Migogoro ya Kikanda"; na ililenga katika kuasisi mifumo ya awali ya ushirikiano kati ya Iran na majirani zake wa Kiarabu.

Duru ya pili ya mkutano huu, pia uliofanyika mjini Doha mwaka 2023, ilifanyika chini ya anwani "Hatua na Njia za Ufumbuzi kwa ajili ya Usalama, Uchumi na Migogoro," ambapo ajenda ya mkutano huo ilipanuliwa kwa kujumuisha mifumo mbalimbali ya ushirikiano wa kivitendo. Duru ya tatu pia ilifanyika hapa Tehran mwaka 2024 chini ya anwani "Mazungumzo kwa ajili ya Ushirikiano na Maelewano" ambapo Iran kwa mara ya kwanza ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Kushiriki Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika "Mkutano wa Nne wa Mazungumzo kati ya  Iran na Nchi za Kiarabu" kunaonyesha mwelekeo wa kidiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni katika nyanja mbalimbali na nchi jirani.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote imekuwa ikionyesha utayarifu na azma yake ya kushirikiana na nchi jirani na haina mipaka katika kushirikiana na nchi za kanda hii, hata hivyo bila ya uingiliaji wa maajinabi.

Maslahi ya Iran na nchi za Kiarabu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kiusalama yanahitaji kuboreshwa na kuimarishwa uhusiano wa pande mbili na wa kieneo, na inaonekana kwamba viongozi wa nchi za Kiarabu pia wako tayari kupanua uhusiano  katika nyanja mbalimbali na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Your Comment

You are replying to: .
captcha